Uhaba wa Dola Wapaisha Bei ya Petroli, Dizeli

Written by on August 2, 2023

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetoa taarifa kwa umma kwa kutangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini Tanzania ambapo bei hizo mpya zimeanza kutumika kuanzia  leo tarehe 5 Julai 2023.

Mamlaka hiyo imetoa bei elekezi kwa Mikoa wa Dar es salaam dizeli ni Tsh 2935 na petrol ni Tsh 3199 kwa lita, vilevile kwa mikoa ya  Kaskazini bei ya rejareja ya mafuta ya petroli imeshuka kwa Shilingi 188/Lita wakati bei ya mafuta ya dizeli imeongezeka kwa shilingi 58/lita. Pia kwa Mikoa ya Kusini bei ya rejareja ya dizeli itaendelea kuwa ni ile iliyotangazwa katika toleo la tarehe 7 Juni 2023.

Hii ni kutokana na kutokuwepo kwa shehena ya bidhaa za mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara pia na kutokana na upungufu wa bidhaa ya petroli katika maghala ya kuhifadhi mafuta yaliyopo Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta wameshauriwa kuchukua mafuta hayo kutoka katika bandari ya Dar es Salaam. Hivyo basi, bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa hiyo zitazingatia bei kikomo ya rejareja ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.
EWURA pia imeeleza mabadiliko hayo ni kutokana na changamoto ya upatikanaji wa dola za marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani pia  ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia sambamba na gharama za uagizaji wa mafuta.

Hivyo basi, kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa zikiwa na  lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.


Current track

Title

Artist