Kaseja afanyiwa upasuaji

Mlinda mlango wa Taifa Stars na klabu ya KMC, Juma Kaseja amefanyiwa upasuaji wa goti jana Disemba 28 kufuatia majeraha aliyoyapata hivi karibuni.

Kaseja alijitonesha majeraha hayo katika kambi ya timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ iliyokuwa ikijiandaa kwa michuano ya CECAFA Senior Challenge Cup mapema mwezi Disemba, ambapo aliachwa kwa matibabu zaidi.

Uongozi wa KMC kupitia kwa Afisa Habari, Anwari Binde umethibisha oparesheni hiyo, “ni kweli Kaseja amefanyiwa upasuaji wa goti jana baada ya kuumia hivi karibuni lakini kwa sasa anaendelea vizuri na tunaamini atarejea tena kwenye kikosi kwa ajili ya kuipigania klabu yetu

Bado hatujapata ripoti ya daktari kwamba Kaseja atatakiwa kupumzika kwa muda gani kabla ya kurudi uwanjani“, ameongeza Binde.

Mechi ya mwisho kwa Kaseja kuichezea KMC ni Novemba 22 kwenye mchezo dhidi ya Alliance FC na baada ya hapo magolikipa Jonathan Nahimana na golikipa namba tatu Denis Richard wakibadilishana nafasi.

Leave a comment