Sabaya Kuendelea Kusota Rumande

Written by on October 12, 2022

Olengai Sabaya

MWENDESHA Mashtaka wa Serikali Kassim Nassir katika kesi uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwa upelelezi wa shauri hilo utakamilika ndani ya siku 90.

Shauri hilo ambalo limetajwa mahakama hapo kwa mara ya 10 sasa bila ya usikilizwaji wake kuendelea kutokana na kile kinachoelezwa na upande wa utetezi kuwa upelelezi kutokamilika .

Mbele ya Hakimu Mfawidhi mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Salome Mshasha Wakili wa upande wa utetezi Hellen Mahuna aliieleza mahakama kuwa kesi inayomkabili mteja wake imekaa siku 132 bila upande wa mashitaka kueleza chochote kinachoeleweka zaidi ya kueleza kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Wakili Mahuna akaiomba mahakama iangalie na itumie hekima na muongozo uliotolewa na Mkurugenzi wa mashitaka nchini( DPP) ya kwamba upelelezi unatakiwa ukamilike ndani ya siku 90.

“Wamekuwa hawakamilishi upelelezi kwa wakati na wanamweka mshatakiwa ndani na kumnyima haki zake za msingi ” alisemaa Mahuna.

Wakili Mahuna aliieleza mahakama hiyo kuwa kama kuna jambo upande wa mashitaka wanatakiwa kulifanya kutokana na mwongozo wa DPP walifanye na wasitegemee kwamba mwongozo umekaa siku 10 tu waangalie siku shauri hilo lilipofikishwa mahakamani.

Wakili Mwandamizi wa Serikali Kassim Nassir aliieleza kuwa, kwa kuwa mwongozo huo umeanza kutumika Oktoba mosi mwaka huu na kwamba ni siku 10 tu zimepita upelelezi wa shauri hilo utakamilika ndani ya siku 90.

Hakimu Mshasha aliiahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba 24 mwaka huu itakapotajwa tena na kwamba mshitakiwa ataendelea kuwa chini ya ulinzi wa magereza akisubiri upelelezi utakapo kamilika.


Current track

Title

Artist